Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Licha ya maelezo na tafsiri nyingi kutolewa, bado swali hili linaibuka tena: “Kwa nini Operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa ilifanyika, au kwa nini ilipaswa kufanyika?” Hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya watu baada ya tarehe 7 Oktoba 2023, waliposhuhudia mauaji makubwa ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, walihoji uhalali wa operesheni hiyo.
Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) – ABNA:
Operesheni Tufani ya Al-Aqsa, iliyoendeshwa na Harakati za Mapambano ya Wapalestina zikiongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023, haikuwa tu kitendo cha kijeshi bali pia nembo ya uamsho wa taifa la Palestina dhidi ya ukaliaji wa mabavu wa utawala wa Kizayuni.
Operesheni hiyo, iliyohusisha uvamizi mkubwa ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kurushwa maelfu ya makombora, ilikuwa matokeo ya miaka mingi ya ukandamizaji, mauaji ya kimbari na uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni unaojiita Israel. Wapalestina, baada ya kuvumilia ukandamizaji wa kimfumo kwa miongo mingi, hawakuona njia nyingine ila mapambano ya kijeshi ili sauti yao isikike duniani.
Historia ya Uvunjaji wa Haki na Haki ya Kujitetea ya Wapalestina
Ukaliaji wa Palestina ulianza mwaka 1948, wakati utawala wa Kizayuni, ukiungwa mkono na nguvu za kikoloni, uliwafukuza mamilioni ya Wapalestina kutoka ardhi zao, tukio linalojulikana kama “Nakba” (Janga). Tangu wakati huo, mauaji ya halaiki, uharibifu wa vijiji, ujenzi wa makazi haramu katika Ukingo wa Magharibi na Quds, pamoja na mzingiro wa Gaza, yamekuwa sehemu ya sera zao.
Ripoti za Umoja wa Mataifa na mashirika kama Amnesty International zinaonyesha kwamba kwa zaidi ya miaka 70, utawala wa Kizayuni umeendelea kukanyaga haki za Wapalestina, ikiwemo kuwakamata watoto, kubomoa nyumba, na kushambulia Msikiti wa Al-Aqsa – alama kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina.
Kwa msaada wa Marekani na Magharibi, Israel imegeuza Palestina kuwa gereza la wazi, huku ikitekeleza siasa za ubaguzi wa rangi (apartheid). Wapalestina walijikuta wakiwa hawana njia nyingine isipokuwa kupigana kwa ajili ya kujilinda.
Kama alivyonukuliwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema:
“Wapalestina wana haki ya kusimama dhidi ya adui aliyenyakua ardhi yao, kuvamia nyumba zao, kuharibu mashamba yao na kuangamiza maisha yao.”
Kwa hivyo, Wapalestina katika Operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa, ingawa walionekana kushambulia, kimsingi walikuwa wanajilinda – jambo ambalo linaungwa mkono na sheria za Kiislamu na hata za kimataifa.
Vichocheo vya Moja kwa Moja: Unyama Uliokithiri na Hali Isiyovumilika Gaza
Miaka michache kabla ya operesheni hiyo, mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi yaliongezeka, na kusababisha vifo vya mamia ya raia. Wakati huo huo, mzingiro wa miaka 16 wa Gaza uliwafunga watu zaidi ya milioni mbili katika umaskini, njaa na mateso makali.
Mwaka 2023, chini ya serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu, Israel iliongeza kasi ya siasa zake za ukandamizaji, ikijaribu kudhibiti kabisa Msikiti wa Al-Aqsa – jambo lililopelekea jina la operesheni hiyo.
Kwa msaada wa Marekani na kimya cha baadhi ya nchi za Kiarabu, Gaza ilibaki gereza kubwa zaidi duniani. Wakati watu wamefungwa bila haki wala matumaini, ni hatua gani nyingine wangechukua zaidi ya kujilinda?
Operesheni hii ikawa mlipuko wa hasira ya miaka mingi ya uvamizi, mauaji na unyanyasaji. Ilikuwa pia ujumbe kwa dunia kwamba Palestina bado ipo na mapambano yanaendelea.
Matokeo na Mafanikio: Kutikiswa kwa Utawala wa Kizayuni na Kuimarika kwa Mhimili wa Mapambano
Miaka miwili baada ya Tufani ya Al-Aqsa (mpaka Oktoba 2025), athari zake zimeonekana wazi. Licha ya mashahidi wengi na vifo vya viongozi wa upinzani kama Yahya Sinwar na Ismail Haniyeh, operesheni hii imeleta ushindi wa kimkakati:
- Dunia imeamka. Wimbi la chuki dhidi ya utawala wa Kizayuni limeenea kutoka Ulaya hadi Marekani.
- Maandamano ya mamilioni yamefanyika kote duniani kupinga mauaji ya Wapalestina.
- Uchumi wa Israel umetikiswa vibaya, bandarini kama Haifa na Eilat zikiathiriwa na mashambulizi ya wanamapambano.
- Harakati za wanafunzi katika vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya zimegeuka kuwa vuguvugu la kimataifa la ukombozi wa Palestina.
- Siasa za “uanzishaji wa uhusiano na Israel” katika nchi za Kiarabu zimesitishwa.
Kiongozi wa Mapinduzi alisema:
“Tufani ya Al-Aqsa na upinzani wa mwaka mzima wa Gaza na Lebanon vimeurudisha utawala wa Kizayuni miaka sabini nyuma – katika hofu ya kuangamia kwake.”
Kwa maneno mengine, siasa za upanuzi za utawala huo zimefikia mwisho; sasa unajitahidi tu kuishi.
Hitimisho: Jibu kwa Historia na Dhamiri za Binadamu
Kwa muda mrefu, Gaza imekuwa katika damu na maangamizi. Lakini historia inatuambia kwamba ushahidi, uharibifu na njaa si ishara ya kushindwa. Bali ni mwanzo wa ushindi wa kimaadili na kiroho.
Operesheni ya Tufani ya Al-Aqsa imeangusha kinyago cha “utawala usioweza kushindwa” na kuufanya utawala wa Kizayuni kuwa chukizo la dunia. Ulimwengu sasa umeamka – kutoka mashariki hadi magharibi, sauti ya uhuru wa Palestina inasikika.
Na bila shaka, uaminifu wa damu za mashahidi na mateso ya wanyonge ndiyo yatakayokuwa nguzo ya uamsho wa mwisho – Uadilifu wa Imam Mahdi (af) – kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Swali la kihistoria tunalotakiwa kulitolea Majibu ya Kihistoria na ya ndani ya nafsi zetu ni hili:
Katika mapambano kati ya jeshi la Mwenyezi Mungu na jeshi la Shetani, sisi tunatakuwa kusimama upande upi?.
Your Comment